'Watanzania endeleeni kuombea taifa’

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuliombea Taifa ili liendelee kudumu katika hali ya amani na utulivu. Alisema suala la kudumisha amani na utulivu ni jukumu la kila mmoja, hivyo kila mwananchi kwa imani yake ahakikishe anashiriki kutunza hali hiyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana baada ya kumaliza kuswali sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Gadaf mjini Dodoma. Alisema ni vema kila mwananchi, akajivunia hali ya amani na utulivu iliyopo nchini kwa kuwa ndiyo inayowezesha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za
kimaendeleo.
“Tuendelee kudumisha amani, tufanye ibada kila mtu kwa imani yake. Serikali inaheshimu dini zote kwa sababu ndizo zinazojenga amani na mshikamano,” alisema. Aliwataka pia wazazi wahakikishe wanawalea watoto wao katika mazingira ya kidini ili wanapokuwa watu wazima waje kuwa raia wema.
Waziri Mkuu aliwakumbusha Waislamu wahakikishe wanautumia vizuri Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuzidisha ibada na kusaidia watu wenye mahitaji. Ibada hiyo ya sala ya Ijumaa iliongozwa na Sheikh Nurdin Kishki, ambaye ni Imamu wa Msikiti wa Vetenari wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Kishki katika hotuba yake, aliwasisitiza Waislamu waendelee kufanya mambo mema yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu ikiwemo kuwatunza wazazi wao, kumswalia Mtume Mohammed (S.A.W) na kufunga katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

www.habarileo.co.tz

Comments