Kambi ya riadha Kenya ilete medali

EBAKI miezi miwili kamili kabla ya kuanza kwa mashindano ya dunia ya riadha jijini London, Uingereza, ambapo Tanzania inataraji kushiriki kama kawaida. Haya ndio mashindano makubwa kabisa ya riadha duniani na huwa na ushindani mkubwa zaidi katika mchezo huo kuliko mengine yoyote. Pia mashindano hayo ni ya tatu kwa ukubwa kwa upande wa ushiriki wa wachezaji wakati ya kwanza ni yale ya Olimpiki nay a pili ni Kombe la Dunia ya soka. Olimpiki ndio michezo mikubwa zaidi inayoshirikisha michezo mingi kwa wakati mmoja, hivyo mashindano hayo ya riadha ya dunia ndio makubwa katika mchezo huo.
MEDALI KATIKA OLIMPIKI
Tanzania ina medali mbili kutoka katika Michezo ya
Olimpiki ilizopata Moscow, Urusi mwaka 1980 kupitia kwa Filbert Bayi na Suleiman Nyambui. Ni miaka 37 sasa tangu Tanzania ilipopata medali hizo za mwanzo na mwisho katika Michezo ya Olimpiki.
Tanzania kwa miaka mingi imekuwa pia ikishiriki mashindano ya dunia ya riadha, lakini imekuja kupata medali hiyo mwaka 2005, yaani miaka 12 iliyopita mashindano hayo yalipofanyikia Helisink, Finland.
Mwanariadha wa Tanzania aliyeleta medali hiyo ni Christopher Isegwe aliyepata medali ya fedha baada ya kumaliza wa pili katika mashindano hayo katika mbio za marathon. Hivyo, pamoja na ukubwa wa Michezo ya Olimpiki, lakini mashindano ya dunia ya riadha ndio mwisho wa matatizo katika mchezo huo kutokana na ushindani na ugumu wake.
Na ndio maana katika miaka yote tangu Tanzania imepata uhuru, ni Isegwe peke yake aliyewahi kutwaa medali katika mashindano hayo ya dunia wakati katika Olimpiki kuna medali mbili.
MIPANGO YA RIADHA TANZANIA
Tayari Riadha Tanzania (RT) imetangaza tarehe rasmi ya kuanza kambi na wanariadha watakaoshiriki, makocha na wapi watakapokaa. Timu ya taifa ya riadha ya Tanzania itapiga kambi nchini Kenya katika eneo linalojulikana kama Iten chini ya makocha, Francis John pamoja na Zacharie Balie.
Wachezaji wanaounda timu hiyo ya Tanzania itakayopiga kambi Kenya ni pamoja na Alphonce Simbu, Said Makula na Ezekiel Ngimba, ambao watashindana katika mbio za marathon wakati Gerald Gabriel amefuzu kushiriki mbio za meta 5,000.
Hata hivyo, Gerald hatakuwemo katika kambi hiyo ya Kenya, ambayo itakuwa pia na wanariadha wawili wakike, Sarah Ramadhani pamoja na Magdalena Shauri ambao ni wakimbiaji wa marathon.
SABABU ZA KWENDA KENYA
Kamati ya Ufundi ya Riadha Tanzania ilikutana jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kuamua kwa kauli moja kuwa, kambi ya timu ya taifa ya Tanzania iwe Kenya ili kupata changamoto zaidi.
Moja ya sababu ya kupeleka kambi hiyo Kenya ni kumuwezesha Simbu angalau kupata ushindani kutoka kwa wanariadha wa Kenya, kwani hapa nchini hana mpinzani. Ofisa Habari wa RT, Tullo Chambo alikaririwa akisema baada ya kikao hicho kuwa, Simbu amekuwa akipata shida kufanya mazoezi, kwani wanariadha anaoshindana nao hawamuwezi kabisa.
Hivyo, ikatumika busara kuamua timu kuipeleka Kenya ili kupata upinzani wa kutosha na aweze kupata kitu kutoka katika mazoezi atakayopewa na Wakenya, ambao wanajulikana kwa makali yao katika marathon.
MAANDALIZI YAMECHELEWA Pamoja na kuchelewa kuanza kwa maandalizi hayo ya mashindano ya dunia ya riadha, lakini sio haba kwani huko nyuma maandalizi yetu yalikuwa ya ubabaishaji zaidi.
Wanariadha wengi huko walikuwa wakijiandaa wenyewe kwa muda mrefu na ukibaki muda mfupi ndio chama kilikuwa kikiwachukua wanariadha hao na kuwaweka pamoja. Hakuna shaka kuwa RT ya sasa inastahili pongezi kwa hili la kuipeleka timu Kenya kwani hiyo ndio inaweza kuwa muarubaini wa kukosa medali katika mashindano ya dunia.
Hakuna ubishi kuwa maandalizi ya mapema na ya uhakika yanasaidia kupatikana kwa matokeo mazuri, ambapo kazi inabaki kwa kujituma kwa wachezaji wenyewe. Kama wanariadha hao wakijiandaa vizuri hakuna ubishi kuwa watafanya ‘maajabu’ katika mashindano hayo ya dunia yatakayofanyika jijini London mwaka huu.


www.habarileo.co.tz

Comments